Maadhimisho ya Mara Day Ushirikiano Wa Tanzania na Kenya Katika Kulinda Mazingira.
Kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa Beatrice Askul ameshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara (Mara Day) yaliondaliwa na Tume ya Bonde la Victoria (Lake Victoria Basin Commission) kwenye uwanja wa Mwenge Wilayani Butiama, Mkoa wa Mara.
Lengo la maadhimisho haya ni kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji na ikolojia ya Mto kwa minajili ya uhai wa jamii na uchumi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rasilimali hii si muhimu tu kwa Mkoa wa Mara na Tanzania, bali pia kwa mamilioni ya viumbe hai wakiwemo wanyama wanaohama kila mwaka kutoka Hifadhi ya Serengeti hadi Maasai Mara nchini Kenya.
Maadhimisho ya mwaka huu ilijumuisha shughuli mbalimbali, ikiwemo upandaji miti katika eneo la bonde la mto Mara, maonesho ya bidhaa za ufundi, michezo na mijadala ya kitaalamu juu ya uhifadhi wa bonde la mto mara na mazingira kwa ujumla.
Kila ifikapo September 15 ya kila mwaka, maadhimisho ya Mara Day huandaliwa kwa kupokezana kati ya nchi za Tanzania na Kenya, zikiwa ni nchi zenye Bonde la Mto Mara na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu katika uhifadhi wa mazingira.
Kwenye ujumbe wa Kenya alikuwemo Waziri wa Maji, Usafi wa Mazingira na Umwagiliaji Eng. Eric Mugaa pamoja na Mh. David Ole Sankok kutoka Bunge la Afrika Mashariki.